Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma – DPP amefunga rasmi kesi ya kwanza ya mauaji ya Shakahola inayomhusisha mhubiri tata Paul Nthenge Mackenzie na washitakiwa wenza 35.
Kesi hiyo, iliyolenga uhalifu dhidi ya watoto, ilihitimishwa jana katika Mahakama ya Watoto ya Tononoka baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa kusikilizwa kwake.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Jami Yamina na kundi la mawakili wakuu, ulianza kuwasilisha ushahidi wake Julai 24, 2024.
Jumla ya mashahidi 76 waliitwa kutoa ushahidi kuhusu mashtaka ya ukatili dhidi ya watoto, mateso na kunyimwa haki ya elimu kuhusiana na matukio yaliyotokea kwenye msitu wa Shakahola.
Ushahidi muhimu katika siku ya mwisho uliwasilishwa na mashahidi watatu, akiwemo mchambuzi wa deta kutoka Safaricom, Dennis Muriithi, ambaye alithibitisha kuwa deta za simu zilihusisha baadhi ya washitakiwa na kesi hiyo.
Msichana aliyenusurika wa umri wa miaka 21, Israel Veronica, alisimulia jinsi babake alimtoa yeye na ndugu zake sita shuleni, akisema elimu ni dhambi, kisha familia ikahamia Shakahola.
Inspekta Phoebe Okomo kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai alielezea jinsi watoto 27 waliokolewa kutoka mazingira hatarishi.
Alisimulia ushahidi wa kutisha kuhusu unyanyasaji, kufunga kwa kulazimishwa na maisha katika maeneo ya mbali yaliyoitwa Yudea, Samaria na Yerusalemu.
Imebainika kwamba baadhi ya watoto walihitaji msaada wa kimatibabu na kisaikolojia.
Kesi imepangwa kutajwa tena Oktoba 14, 2025, ili kuthibitisha iwapo kumbukumbu za mashauri zimeandikwa kwa ajili ya uwasilishaji wa hoja.
Mackenzie na wenzake pia wanakabiliwa na mashtaka mengine ya mauaji, kuua bila kukusudia na ugaidi katika mahakama tofauti.