DPP aagiza Gavana wa Isiolo Abdi Ibrahim akamatwe

Tom Mathinji
2 Min Read
Abdi Guyo, Gavana wa kaunti ya Isiolo

Kiongozi wa Mashtaka ya Umaa (DPP)), ameagiza Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kumkamata Gavana wa kaunti ya Isiolo Ibrahim Abdi Hassan, almaarufu  Guyo, pamoja na watu wengine saba, kwa madai ya kuhusika katika utekaji nyara na wizi wa kimabavu.

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa Ijumaa, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma alisema hatua hiyo imeafikiwa baada ya uchunguzi wa kina wa kesi iliyowasilishwa na maafisa wa DCI eneo la Kiyumbi kwa afisi ya DPP kaunti ya Machakos, na baadaye ikihamishwa hadi Makao Makuu Jijini Nairobi kutokana na umuhimu wake.

Kulingana na taarifa hiyo, aliyekuwa Waziri wa Afya wa kaunti ya Isiolo  Abdirahaman Mohamed, na wanachama wengine 15 wa bunge la kaunti ya Isiolo waliokuwa wakishinikiza kuondolewa mamlakani kwa Gavana Guyo, walikuwa wakishiriki mkutano katika hoteli ya Outbark iliyoko Maanzoni, kaunti ya Machakos.

Ripoti hiyo inadokeza kuwa Gavana Guyo na wafuasi wake walivamia hoteli hiyo, huku kupitia amri za Guyo, wafuasi hao walimshambulia Abdirahaman, kabla ya kumlazimisha kuabiri gari na kumteka nyara.

Taarifa hiyo ya DPP, ilisema Gavana huyo alimtishia afisa huyo wa zamani na kuwalazimisha wafuasi wake kumpeleka katika eneo la Ruai alikochapwa na kuachwa.

Wakati wa purukushani hiyo,  Abdirahaman alipoteza bastola yake aina ya Glock ikiwa na risasi 15, simu aina ya iPhone 16, shilingi 70,000 pesa taslimu na vitu vingine vya kibinafsi.

Kamera fiche za CCTV zilithibitisha kuwa Gavana huyo alikuwa katika eneo la mkasa akiwa pamoja na Abdullahi Jaldesa Banticah, Dade Boru, Abdirashid Ali Diba almaarufu Ngila, Abdinur Dima Jiilo, Ahmed Duale, Josephat Mwangi Komu, na Yusuf Maina.

Kiongozi wa Mashtaka ya umma ameagiza washukiwa hao wafikishwe mahakamani wafunguliwe mashtaka ya utekaji nyara kwa lengo la kusababisha maejara na wizi wa kimabavu.

Share This Article