Douglas Kanja ameapishwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi, saa chache baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu katika wadhifa huo.
Hafla ya kumuapisha iliongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome leo Alhamisi katika majengo ya idara ya mahakama jijini Nairobi.

Gilbert Masengeli ambaye amekuwa akikaimu wadhifa huo na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI Mohamed Amin ni miongoni wa waliohudhuria hafla hiyo.

Kwa kipindi ambacho Masengeli amehudumu kama kaimu IG, amekumbana na mawimbi makali ya kisheria.
Jaji Lawrence Mugambi amemhukumu kifungo cha miezi sita jela kwa kuidharau mahakama, kifungu kinachoweza kuanza kutekelezwa kesho Ijumaa.
Juhudi za Masengeli kutaka kifungu hicho kuahirishwa hazijafua dafu.
Wadhifa wa Inspekta Jenerali wa Polisi ulisalia wazi kufuatia kujiuzlu kwa Japhet Koome mwezi Julai mwaka huu.