Don Richard asimulia kuhusu matatizo ya kiafya

Richard alikumbwa na matatizo ya kiafya baada ya kuacha kutumia pombe na sigara, wakati alidhania atakuwa na afya bora.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa Nollywood nchini Nigeria Richards Oguntimehin maarufu kama Don Richard amesimulia kuhusu tatizo la kiafya lililomkumba ghafla baada ya kuamua kuacha kutumia pombe na sigara.

Msanii huyo alionekana kwenye video ambapo alikiri kwamba alianza kupata matatizo makubwa kiafya miaka miwili tu baada ya kuacha mtindo wake wa awali wa maisha.

Mshutuko wa kuwa mgonjwa wakati alitarajia kuwa na afya bora, anasema ilifanya hali iwe ngumu hata zaidi. Alilazwa hospitalini na anasema tukio hilo lilimsukuma afikirie sana kuhusu chaguo la mtindo wa maisha.

Mwigizaji huyo anasema ni katika kitanda cha hospitali ambapo aligundua kitu ambacho watu wengi hawajui: kwamba magonjwa mengi yanayoua watu ni ya ndani na mara nyingi dalili huwa hazionekani kwa nje.

“Athari zilikuwa zimejikusanya kwa miaka kadhaa… viungo kushindwa kufanya kazi sio jambo la ghafla … ni mkusanyiko wa tabia zako … kuacha tabia hizo ghafla hakumaanishi madhara hayakuwa yamefanyika” alisema mwigizaji huyo.

Don Richard aliingilia tasnia ya burudani miaka ya 80 akianzia katika kituo cha runinga cha NTA 10, ambapo alijifunza mengi kuhusu burudani na maandalizi ya vipindi.

Anasema alianza kazi kama mwigizaji lakini Danladi Bako, akamfungua macho akafahamu kwamba alikuwa na uwezo katika maandalizi na maelekezi.

Tangu wakati huo, Don Richard amehusika katika maandalizi ya filamu kadhaa za Nollywood zikiwemo za lugha ua Igbo.

Share This Article