Diva Thee Bawse aondoka Wasafi Fm

Alitangaza hatua hiyo kupitia Instagram na kwenye kikao na wanahabari leo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtangazaji wa redio nchini Tanzania Diva Gissele Malinzi maarufu kama Diva Thee Bawse ametangaza rasmi kwamba ameondoka kwenye kituo cha redio cha Wasafi FM baada ya miaka minne.

Diva ambaye amekuwa akitangaza kwenye kipindi cha usiku cha Lavidavi alitoa habari hizo kupitia ujumbe aliochapisha kwenye akaunti yake ya Instagram asubuhi akithibitisha kwamba aliwasilisha barua ya kujiuzulu.

Alishukuru watu wa familia ya Wasafi Media na mashabiki wake ambao wamemfuatilia kwa kipindi chote cha miaka minne na kuongeza kwamba kipindi cha Lavidavi ni sura nzuri zaidi katika kazi yake.

“Tulijenga nyumba ya simulizi za mapenzi, uponyaji, kicheko na mazungumzo ya kweli. Kila sauti, kila ujumbe, kila usiku – mmekuwa sehemu ya moyo wangu” aliandika Diva.

Akizungumza na wanahabari baadaye, mtangazaji huyo hata hivyo alilalamika kuhusu hatua ya Wasafi TV kumhoji Ruta Bushoke akielezea kwamba alihisi kudhalilishwa.

Diva aliwahi kuwa mwenyeji wa mwanamuziki Bushoke kwenye studio za Wasafi Fm ambapo alikuwa akimhoji lakini hakufurahishwa na jinsi alikuwa anajibu maswali yake.

Mtangazaji huyo alikasirika pale ambapo Bushoke alikosa kubadili maongezi yake na akalazimika kukatiza mahojiano hayo. Baadaye Bushoke alihojiwa kwenye kipindi kingine cha Wasafi Fm ambapo Diva anahisi aliongelelewa vibaya.

Leo Diva amemshauri Bushoke aangazie mambo bora zaidi badala ya kuendelea na mahojiano kwenye vyombo vya habari akimsema.

Diva Thee Bawse hata hivyo anasisitiza kwamba hajakosana na mmiliki wa Wasafi Media Diamond Platnumz akisema anampenda sana.

Share This Article