Diddy aomba kesi yake isimamishwe

Ombi lake linatokana na uwezekano wa kuondolewa kwa mmoja wa waamuzi wa kesi hiyo aliyetoa taarifa kinzani kuhusu makazi yake.

Marion Bosire
1 Min Read
Sean "Diddy" Combs

Msanii wa muziki nchini Marekani P.Diddy kwa mara nyingine ameomba jaji anayesikiliza kesi inayomkabili aisimamishe kufuatia hatua yake ya kuondoa mmoja wa waamuzi wa kesi hiyo.

Ijumaa jaji Arun Subramanian alitangaza mipango ya kumwondoa mmoja wa waamuzi kufuatia hatua yake ya kutoa maelezo yaliyokinzana kuhusu anakoishi.

Diddy sasa analaumu waendesha mashtaka katika kesi yake kwa kujaribu kuondoa mwamuzi mweusi akitaka kesi hiyo isimamishwe iwapo jaji ataafikia uamuzi wa kutimu mwamuzi huyo.

Jumapili mawakili wa Diddy walimwandikia jaji Arun Subramanian waraka wakielezea kwamba hata ingawa mahakama inakubaliana na waendesha mashtaka waliokosa imani na mwamuzi huyo, serikali inasingizia hilo kumtimua kutokana na rangi yake ya ngozi.

Kundi la Diddy linahisi kwamba majibu kinzani ya mwamuzi huyo kuhusu makazi yake hayamaanishi kwamba hatoshi kuhudumu kwenye kundi la waamuzi, wakinukuu matamshi ya jaji kwamba suala hilo halihusiani na uwezo wake wa kufanya maamuzi.

Diddy anasisitiza kwamba iwapo mwamuzi huyo atatimuliwa basi anafaa kupata ombi lake la kusimamishwa kwa kesi hiyo ili kuruhusu uteuzi mpya wa kundi la waamuzi.

Hii ni mara ya tatu Diddy anaomba kesi dhidi yake isimamishwe kupitiwa kwa wakili wake Xavier Donaldson, huku maombi yake mawili ya awali yakitupiliwa mbali.

Share This Article