Diddy ahukumiwa miezi 50 gerezani

Marion Bosire
2 Min Read
P Diddy

Mwanamuziki na mfanyabiashara wa muda mrefu nchini Marekani Sean “Diddy” Combs, amehukumiwa kifungo cha miezi 50 gerezani sawa na miana minne na miezi miwili, kutokana na hatia aliyopatikana nayo kwenye makosa mawili ya usafirishaji wa binadamu kuwatumia kingono.

Jaji Arun Subramanian alitoa uamuzi huo Ijumaa Oktoba 3, 2025 ambapo alisema kifungo kikubwa kilistahili kutolewa ili kutuma ujumbe kwa wanaodhulumu wengine kingono na wanaodhulumiwa.

Ujumbe huo kulingana na Subramanian ni “Dhuluma dhidi ya wanawake hukabiliwa na uwajibikaji wa ukweli”.

Jaji huyo alisema pia kwamba wakati huu ni mgumu kwa Combs na familia yake lakini atakuwa na maisha baada ya kifungo hicho.

Combs alihakikishiwa kwamba mahakama imekubalia huduma za matibabu lakini sio za kulazwa hospitalini na anakubaliwa pia kupokea huduma za ushauri nasaha.

Baada ya kifungo hicho cha gerezani, Jaji Subramanian aliagiza kwamba Combs afuatiliwe kwa muda wa miaka mitano zaidi.

Mawakili wa Combs walikuwa wamemtetea mahakamani kabla ya uamuzi huo kutolewa wakitaka aachiliwe mara moja na Jaji asimhukumu kifungo kinachozidi miezi 14, muda aliokaa kizuizini ukujumuishwa.

Waendesha mashtaka kwa upande mwingine walikuwa wameomba mahakama itoe hukumu ya kifungo cha zaidi ya miaka 11 gerezani.

Combs alipatikana na hatia katika makosa mawili ya kusafirisha watu kwa ajili ya kuwatumia kwenye biashara ya ngono mwezi Julai ila aliondolewa makosa makubwa ya kingono ya usafirishaji wa watu na kushirikiana na wengine kupanga na kutekeleza uhalifu.

Makosa hayo yana adhabu ya hadi kifungo cha maisha gerezani.

Share This Article