Diana Marua mke wa mwanamuziki Kevin Kioko maarufu kama Bahati ametoa taarifa kwa umma kuhusu muziki ambao Bahati ameamua kufanya sasa.
“Ninajua wengi wenu mmeona minong’ono na maudhui kuhusu Bahati” alianza taarifa yake Marua akiongeza kwamba hata ingawa anaheshimu safari ya mume wake kama mwanamuziki na maamuzi anayofanya angependa kufafanua kuhusu msimamo wake.
Alijitenga na mtindo mpya wa Bahati katika muziki akisema kwamba malengo yake ni tofauti akisema anaangaziabiashara zake, mikataba yake na kampuni mbali mbali na nembo zinazomwamini.
“Hii inamaanisha kwamba ninajibeba kwa njia inayodhihirisha wajibu wake, ukuaji na maadili ninayosimamia.” Aliendelea kusema mama huyo ambaye pia ni mwanamuziki.
Marua alisema kutokana na heshima aliyonayo kwa familia yake, washirika na watu wanaomtizamia hatajihusisha na mtindo mpya wa Bahati katika muziki.
“Ninaamini katika kusaidiana lakini pia ninaamini katika kulinda nembo yangu na nafasi ambazo ninajenga” alimalizia Diana Marua akishukuru wafuasi wake na kampuni anazoshirikiana nazo.
Marua anaonekana kuchukua hatua hii kama mkakati wa kulinda mikataba yake na kampuni anazoshirikiana nazo hasa katika kutangaza bidhaa zao kufuatia video zilizosambaa mitandaoni za muziki mpya wa Bahati.
Katika video hiyo, Bahati anaonekana akiwa ameketi akiimba huku akichezewa kwa karibu na mwanadada aliye na makalio makubwa na ambaye hana mavazi ya heshima.