Diamond na Zuchu wafunga ndoa

Picha na video za tukio hilo zimesambazwa mitandaoni hata na wahusika wenyewe.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Naseeb Abdul Juma maarufu kama Diamond Platnumz na mwenzake Zuhura Othman maarufu kama Zuchu wamefunga ndoa.

Haya ni kulingana na video na picha zinazosambaa mitandaoni zinazowaonyesha wawili hao wakifunga ndoa kwa mujibu wa taratibu za kiisilamu nyumbani.

Diamond naye alichapisha picha ambazo hazionyeshi vizuri uso wa anayemwoa akikiri kufunga ndoa japo si moja kwa moja, lakini chapisho la mamake mzazi linathibitisha kwamba ni Zuchu.

Katika chapisho lake, Diamond kwa maneno mengi alielezea jinsi amejifunza kutotangaza mambo yanayoendelea kwenye maisha yake akisema tabia hiyo imemletea amani.

“Najua kila mmoja wenu ana picha tofauti kabisa kuhusu Diamond Platnumz na KUOA,” aliandika mwanamuziki huyo na kumalizia kwamba “ila tu nataka leo niwaambie kuwa HUYU DIAMOND PLATNUMZ ALISHAWAHI KUOA, na kuna siku nitawaambia ikawaje.”

Mamake ambaye hujiita Mama Dangote kwenye Instagram alichapisha video inayomwonyesha Diamond akiwa ameketi na Shehe wakiendeleza taratibu za ndoa na kuandika, “Alhamdullillah limepita salama. Hongera mwanangu Naseeb kichwa na mkeo Zuhura”.

Mange Kimambi ambaye anaendesha mtandao wa habari naye alikuwa amekiri awali kupokea ripoti kutoka kwa watu tofauti kuhusu ndoa ya Diamond na Zuchu pamoja na ithibati.

Juma Jux ambaye ameoa hivi maajuzi naye alimwandikia Diamond, “Karibu kwenye kundi kaka”.

Share This Article