Diamond awataka Mbosso na Levo wamheshimu

Hii ni baada yake kutajwa na Baba Levo kwenye ugomvi aliozua kuhusu wimbo wa Mbosso uitwao Pawa.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Tanzania Abdul Naseeb maarufu kama Diamond Platnumz ametumia Instagram kuwasilisha ujumbe wake kwa msanii mwenza Mbosso na mtu wake wa karibu Baba Levo.

“Baba Levo Wewe ni kijana mwenzangu na naheshimu nafasi yako ila unapoelekea unanilazimisha kukaa mbali na wewe maana unafanya nihisi kuna agenda nisiojua unanitengenezea” aliandika Diamond akirejelea ugomvi alioanzisha Baba Levo kuhusu wimbo ‘Pawa’ wa Mbosso.

Baba Levo alikuwa amechapisha jumbe kadhaa kwenye Instagram akisema kwamba Diamond alichangia pakubwa katika maandalizi ya wimbo huo lakini Mbosso hana shukrani.

Kwa Mbosso Diamond aliandika, “Una haki ya kutopendezwa, kuchukia na kureact kwa namna yoyote unayohisi ni sahihi unapokosewa ila naomba usinijumuishe kwenye ujinga wa baba levo na nadhani tushaliongea hili si mara moja wala mbili tena kwa ushahidi na mifano”.

Mwanamuziki huyo alihimiza wawili hao wamheshimu vile anawaheshimu lakini iwapo kuna ajenda wanayotaka kuendeleza kupitia kivuli chake bila yeye kujua, amewahimiza waendelee.

Mbosso naye alitumia Instagram kumjibu Diamond ambaye alikuwa msimamizi wake alipokuwa kwenye kampuni ya wasafi akisema yeye ndiye mtu sahihi wa kumkanya Baba Levo ikitizamiwa ukaribu wao.

“Mimi na Baba Levo Wapi na Wapi, Hatukutani , Hatufanyi Kazi Pamoja, hatushindi Pamoja na Wala Hatusafiri Pamoja .
Tusizunguke Mbuyu.. Mtu Pekee Wa Kumkanya Baba Levo ni Wewe Bro Sio Mimi ..” aliandika Mbosso akimwelekezea Diamond.

Msanii huyo aliendelea kuhakikishia Diamond kwamba kamwe hawezi kumvunjia heshima kwani anatambua mchango wake mkubwa kwenye maisha yake na hatua alizopiga kama msanii.

Share This Article