Mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz alikuwa nchini Uganda ambapo alitoa ushauri kwa wasanii wa taifa hilo jirani.
Nyota huyo wa Bongo Flava alisema wasanii wa Uganda ni lazima wakatae kutumia ushawishi wao mkubwa waliopata kwa juhudi nyingi kuendeleza kampeni mbali mbali kwa malipo duni au bila malipo.
Diamond ambaye alitumbuiza katika tamasha la Kahawa katika kituo cha Africa Coffee Park, alisema wanamuziki hunyanyaswa ili kupatiwa nyadhifa zisizo na maana kama mabalozi wa nia njema.
Alilalamikia hatua ya baadhi ya serikali ya kutafuta wasanii nje ya mataifa yao wakipuuza wasanii wa nyumbani. Kulingana naye wasanii hutekeleza jukumu muhimu la kusambaza jumbe na ushawishi wao haufai kupuuzwa.
“Serikali na mashirika lazima waanze kutambua wasanii wa nyumbani. Huu sio wakati wa kwenda nje kutafuta watu wenye ushawishi mkubwa kama wacheza soka. Ni lazima watutumie kuafikia malengo yao.” alisema Diamond.
Aliendelea kusema kwamba anaamini viongozi serikalini hawatekelezi shughuli za usaidizi wa jamii, huwa kuna bajeti katika kila shughuli.
“Kazi yetu kama wasanii huhitaji uwekezaji wa kiwango cha juu ndiposa tupate ushawishi tulionao kiasi kwamba wanataka kututumia kuwasilisha jumbe zao” alimalizia.