Msanii wa muziki nchini Tanzania Diamond Platnumz ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya kusimamia wasanii ya Wasafi ametangaza kwamba hajateua msemaji wa maisha yake.
“Onyo! Sijateua yoyote kuwa msemaji wa career ama maisha yangu, hivyo lolote litalozungumzwa na yoyote kuhusu mimi, eidha na alie karibu nami ama asie na ukaribu, naomba lipuuzwe na lisiaminiwe!” aliandika Diamond kwenye tangazo hilo.
Mwanamuziki huyo aliendelea kusema kwamba atakapotaka kutoa taarifa au ujumbe wowote kuhusu maisha yake atasema mwenyewe huku akionya umma dhidi ya kuamini mambo yanayosemwa mitandaoni.
Tangazo hilo alilotoa kupitia Insta Stories linafuatia madai yaliyoibuliwa na Baba Levo ambaye ni mtu wake wa karibu kuhusu aliyekuwa msanii wa Wasafi Mbosso.
Baba Levo alichapisha taarifa ambayo wadadisi wanahisi kwamba ililenga kuharibu uhusiano kati ya Diamond na Mbosso ikitizamiwa kwamba Diamond alimsifia sana Mbosso na kumwachilia kutoka Wasafi bila kumlipisha ada yoyote.
Kulingana na Levo, Diamond alichangia pakubwa wimbo unaovuma sana sasa hivi wa Mbosso uitwao “Pawa” na Mbosso hajaonyesha shukrani kwa Diamond.
Aliambatanisha madai yake na video inayoonyesha Diamond, Mbosso na wengine wakiwa studioni wakati wa maandalizi ya ngoma hiyo ambapo Diamond anaonekana kumwelekeza Mbosso jinsi ya kuimba.
Levo naye amechapisha ujumbe huo wa Diamond wa kufafanua kwamba hana msemaji hatua inayokanganya wengi wasijue iwapo ulimlenga yeye.