Diamond akanusha madai kwamba ameongeza mke

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki nyota nchini Tanzania Diamond Platnumz amekanusha madai kwamba ameongeza mke mwingine, miezi michache tu baada ya kufunga ndoa ya mkeka na mwanamuziki mwenza Zuchu.

“Naona Kuna Misumari inapigiliwa kuwa Simba kaongeza mke, hapana jamani sijaongeza” aliandika mwanamuziki huyo chini ya picha kadhaa alizochapisha kwenye Instagram.

Picha hizo zinaaminika kupigwa wakati wa maandalizi ya video ya muziki ikiwemo moja aliyopigwa na mwanamke mrembo.

Aliendelea kuwasihi wafuasi wake mitandaoni wasimpe ujasiri asiokuwa nao, akionekana kuzungumzia ujasiri wa kuongeza mke mwingine hata ingawa dini yake inamkubalia kuoa hadi wanne.

Msanii huyo alifafanua kuhusu video iliyosambaa mitandaoni akisema, “Clip nyingine inasambaa niko kwa gari na msichana, hiyo ni video yangu nyingine ambayo pia inatoka karibuni”.

Msanii huyo alimalizia kwa kuhakikishia mashabiki wake kwamba mwezi huu wa Oktoba ambao ndio wake wa kuzaliwa ni “Mwezi wa Raha na Burudani tu” na hataki ugomvi na mke wake.

Diamond alifunga ndoa na Zuchu katika hafla ya faragha kunako mwezi Aprili mwaka huu wa 2025, lakini wakaja kufichua hayo mitandaoni mwezi Juni.

Share This Article