Wanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya wasichana ya Alliance almaarufu AGHS, leo waliandamana nje ya lango kuu la taasisi hiyo ya elimu kufuatia madai ya mwalimu wa kiume ambaye amekuwa akidhulumu wanafunzi.
Mwenyekiti wa shirika la walimu na wazazi wa shule hiyo, amethibitisha kwamba wameunda kamati ya muda kwa ushirikianao na chama cha walimu wa shule za sekondari na taasisi za elimu ya juu KUPPET, wizara ya elimu na chama cha wanafunzi wa zamani.
Kamati hiyo imetwikwa jukumu la kuchunguza madai yaliyoibuliwa na wanafunzi kadhaa wa zamani dhidi ya mwalimu aitwaye Peter Ayiro ambaye amefunza katika shule hiyo kwa miaka 25.
Ripoti ya kamati hiyo ya muda inatarajiwa kutolewa kufikia mwisho wa juma lijalo.
Wakili wa chama cha wanafunzi wa zamani wa shule ya wasichana ya Alliance Zahra Nechesa na waliomaliza masomo mwaka 2010 kutoka taasisi hiyo, wameahidi kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya usimamizi wa shule hiyo.
Wanalaumu usimamizi huo kwa kumlinda Ayirotangu mwaka 2011 kwa lengo la kulinda sifa za taasisi hiyo ya elimu.
Madai dhidi ya Ayiro yalisambaa mitandaoni kufuatia ripoti ya mwanahabari na mwanafunzi wa zamani wa AGHS Christine Mungai ambaye alisema kwamba alihoji wanafunzi kadhaa wa zamani waliokiri kudhulumiwa kingono na mwalimu Ayiro.