Idara ya upelelezi wa jinai DCI imetoa taarifa kuhusu kukamatwa kwa mwanaharakati Boniface Mwangi aliyetolewa nyumbani kwake huko Lukenya kaunti ya Machakos jana Jumamosi Julai 19, 2025.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye akaunti rasmi za DCI kwenye mitandao ya kijamii, idara hiyo inaelezea kwamba Mwangi anahusishwa na uwezeshaji wa vitendo vya kigaidi wakati wa maandamano ya Juni 25, 2025.
“Wakati wa kukamatwa kwake, maafisa walichukua simu mbili za rununu, kipakatalishi na vitabu kadhaa vya kuandika” ilisema taarifa hiyo ya DCI.
Wapelelezi hao wanasema kwamba baada ya kumaliza kutoka nyumbani kwake, walimpeleka Mwangi kwenye afisi yake katika jumba la Mageuzi Hub kwenye barabara ya Rose Avenue mtaani Hurlingham.
Baada ya kusaka afisi hiyo, maafisa hao waliondoka na diski tisa za kuhifadhi deta, vipatakalishi viwili, sili za kampuni za Brave Media na Courage, muhuri wa kampuni, vitabu sita vya hundi, nakala za hati za ushuru, makopo mawili ya gesi ya kutoza machozi na vingine.
Mwangi anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Pangani na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho Jumatatu.