Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imeimarisha vita dhidi ya ulanguzi wa binadamu baada ya kutia saini Mkataba wa Maelewano na Taasisi ya Kukabiliana na Ulanguzi wa binadamu (HTI).
Kulingana na DCI, mkataba huo na HTI uliotiwa saini katika Makao Makuu ya DCI Jijini Nairobi, unalenga kukabiliana, kuchunguza na pia kuzuia visa vya ulanguzi wa binadamu hapa nchini.
“Ushirikiano huo unalenga kuzuia, kuchunguza na kukabiliana na ulanguzi wa binadamu kupitia ushirikiano katika ugawanaji habari, mipango ya uhamasishaji na usaidizi wa kiufundi,” ilisema DCI kupitia ukurasa wa X.
Huku akielezea kujitolea kwa DCI katika ushirikiano huo, Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin, alishukuru Taasisi ya HTI kwa ushirikiano huo, akidokeza kuwa ushirikiano huo umejiri wakati ambapo kanda hii inashuhudia ongezeko la visa vya ulanguzi wa binadamu.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais anayehusika na mipango katika taasisi ya HTI J. Tyler Dunman, alisema taasisi hiyo itahakikisha inatekeleza wajibu wake jinsi yalivyoratibiwa kwenye makubaliano hayo.