DCI yaanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya wakili Kyalo Mbobu

Marion Bosire
2 Min Read

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya wakili mashuhuri wa Nairobi, Kyalo Mbobu, aliyeuawa kwa kupigwa risasi yaliyotokea jana Septemba 9, 2025, kando ya barabara ya Magadi.

Katika taarifa iliyotolewa leo, DCI imeelezea masikitiko yake na kutuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki na wenzake marehemu.

Idara hiyo imethibitisha kuwa maafisa wa upelelezi wakiongozwa na mkuu wa upelelezi wa eneo la Nairobi walifika haraka katika eneo la tukio mara baada ya kupokea ripoti.

Wataalamu kutoka kitengo cha mauaji katika DCI kwa kushirikiana na wanasayansi wa Maabara ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Kisayansi walikagua eneo la tukio na kukusanya ushahidi muhimu utakaosaidia katika uchunguzi.

Wananchi wamehakikishiwa kwamba rasilimali zote na utaalamu zinatumika kuhakikisha waliohusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Tumejizatiti kuhakikisha waliohusika na tukio hili la kinyama wanakamatwa na kuwajibishwa ” ilisema taarifa hiyo ya DCI. “Wapelelezi wetu wanaendelea kuchunguza kwa kina matukio yaliyopelekea mauaji haya” iliendelea kusema.

DCI imetoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na kushirikiana na vyombo vya usalama wakati huu.

Yeyote aliye na taarifa kuhusu tukio hilo anaombwa kuwasiliana na kituo cha polisi kilicho karibu, kupiga simu isiyotozwa malipo nambari 0800 722 203 au kutuma ujumbe kupitia WhatsApp kwa nambari 0709 570 000.

Share This Article