Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, imeanzisha uchunguzi kuhusu ghasia zilizozuka wakati maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi EACC, walipozuiwa kutekeleza majukumu yao rasmi katika kaunti ya Trans Nzoia.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema maafisa hao wa EACC walikuwa wakichunguza madai ya ufisadi katika serikali ya kaunti ya Trans Nzoia, yanayodaiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 na 2024/2025.
Serikali ya kaunti ya Trans Nzoia inadaiwa imefuja shilingi bilioni 1.4 kupitia ukiukaji wa sera za ununuzi na malipo ya kutiliwa shaka.
Operesheni ya maafisa hao, ililenga makazi na afisi za Gavana wa kaunti hiyo George Natembeya, pamoja na watu wengine wanne ambao wamehusishwa na kesi hiyo.
Hata hivyo, msako kwenye makazi ya Gavana huyo ulitekelezwa mbele ya familia yake, mwanasheria mkuu wa kaunti na mawakili.
Kizaazaa kilizuka wakati kundi la watu lilipoingia kwa nguvu katika makazi hayo na kuwashinda nguvu maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda zoezi hilo.
Watu hao walizua rabsha na kuharibu magari ya maafisa wa EACC na kuiba vitu na vifaa kwenye magari hayo.
“Ghasia hizo ni juhudi za kuhujumu utekelezwaji wa haki,” ilisema DCI kupitia kwa taarifa.
Idara hiyo ilisema imeanzisha uchunguzi kuhusiana na shamulizi hilo na kuwakamata wahusika.