Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, imeanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha kasisi John Maina wa kanisa katoliki Parokia ya Igwamiti, Nyahururu kaunti ya Nyandarua.
Kulingana na ripoti, mnamo Aprili 27, 2025, kasisi Maina alihudhuria ibada ya kuadhimisha miaka 25 ya kanisa katoliki la Igwamiti pamoja na kutawazwa kwa kasisi Simon Thuita, sherehe iliyohudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na wanasiasa wengine.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema mnamo Mei 15, 2025, msamaria mwema alimpata kasisi Maina kwenye barabara kuu ya Nakuru – Nairobi akiwa na majeraha upande wa kushoto wa kichwa chake.
Msamaria huyo mwema alimpeleka katika hospitali ya St. Joseph Gilgil ambako alianza kupokea matibabu, lakini alifariki dakika chache baada ya kulazwa hospitalini humo.
DCI ilisema uchunguzi wa awali uliashiria kuwa kasisi Maina alikuwa akiandamwa na watu wasiojulikana waliotaka wapewe sehemu ya fedha ambazo zilitolewa na Gachagua wakati wa ibada hiyo.
Watu kadhaa wameandikisha taarifa kuhusu mauaji hayo, huku idara hiyo ikitoa wito kwa walio na habari zitakazosaidia kwa uchunguzi, kuzitoa katika kituo cha polisi kilicho karibu.
“Maafisa wetu wamejitolea kuchunguza mauaji haya kuhakikisha haki inapatikana na kuchukuliwa hatua kwa waliotekeleza,” ilisema DCI.