Mwanamuziki wa Uganda Dax Vibez amezungumzia uhusiano wake wa sasa na rais wa shirikisho la wasanii wa Uganda – UNMF Eddy Kenzo, akifichua kuwa hawazungumzi tena.
Vibez hata hivyo amefafanua kwamba hawajatofautiana kutokana na mgogoro wa kibinafsi bali ni kwa tofauti za kimawazo.
Katika mahojiano, Dax alisema amesikitishwa na mwelekeo ambao Kenzo amechukua, hasa kuhusiana na kujiunga kwake na serikali ya sasa na anavyoshughulikia masuala ya tasnia ya muziki kupitia UNMF.
“Silaumu UNMF kwa kile wanachofanya, ninawalaumu kwa kile ambacho hawafanyi kwa sababu hakuna chochote kinachofanyika. Kenzo alikuwa rafiki yangu wa karibu, lakini mawazo yalibadilika.” Alisema mwanamuziki huyo ambaye ni kaka mdogo wa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine.
Licha ya tofauti zao, Dax anasisitiza kuwa hana chuki na bosi wa Big Talent, akimtambua Kenzo kama msanii mkongwe katika tasnia na mtu muhimu katika safari yake ya muziki.
“Katika muziki, ananiunga mkono. Najua ni shabiki wangu na hata aliwahi kunipigia simu zamani akaniambia anaamini nitakuwa mtu wa kipekee. Ni miongoni mwa wasanii wa kwanza waliokubali kufanya kazi na mimi, ingawa haikuwahi kutoka” aliendelea kusema msanii huyo.
Kulingana na Dax, utengano wake na Kenzo umetokana na kile anachokiona kama usaliti wa maadili na imani ambazo waliwahi kujadili na kuamini pamoja.
“Kwa upande wa mawazo, tulizungumza mambo fulani miaka iliyopita, na sasa naona ametenda kinyume na kile alichokuwa ananifundisha” alielezea.
Wadadisi hata hivyo wanahisi kwamba tofauti kati ya wawili hao inatokana na miegemeo ya kisiasa.