Msanii wa muziki nchini Nigeria David Adeleke, maarufu kama Davido, amelalamikia kile anachokitaja kuwa kunyanyaswa na walinzi wazungu katika kisiwa cha Ibiza nchini Uhispania.
Davido amekuwa akichapisha video za matukio kutoka Ibiza ambapo amekwenda kwa likizo huku wakijiandaa kwa harusi ya meneja wake Asa, ambapo alionekana akiwa na furaha.
Lakini furaha yake ilikatizwa ghafla pale alipochapisha picha za walinzi hao akisema walimdhalilisha ila hakutoa maelezo ya ndani kuhusu tukio hilo.
“Walinzi wamejaribu kuniua pamoja na wasaidizi wangu,” aliandika Davido katika chapisho moja na katika jingine akasema walinzi hao watachukuliwa hatua kali.
Machapisho ya nyota huyo wa muziki wa Afrobeat yamepokelewa kwa njia tofauti na mashabiki wake. Wapo wanaomuunga mkono kuhusiana na lalama zake huku wengine wakimkashifu.