Dar es Salaam yapokea wageni kwa ajili ya harusi ya Juma Jux

Msanii wa Kenya Bahati na mke wake Diana wanawakilisha Kenya katika hafla hiyo ya kesho.

Marion Bosire
2 Min Read
Juma Jux na Priscilla Ojo

Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, limepokea wageni wengi hasa kutoka Nigeria ambao wako huko kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya mwisho ya ndoa ya msanii Juma Jux na Priscilia Ojo wa asili ya Nigeria.

Msanii wa muziki nchini Kenya Kelvin Bahati na mke wake Diana wako Dar es Salaam kuhudhuria hafla hiyo itakayoandaliwa kesho Mei 28, 2025 katika ukumbi wa Superdome.

Wawili hao walichapisha picha za pamoja zinazowaonyesha wakishuka ndege jijini Dar na kuandika, “Tuko Tanzania kusherehekea upendo. Tunawakilisha Kenya kwenye #JP2025”.

Mwigizaji na mwandalizi wa filamu maarufu nchini Nigeria Funke Akindele naye alinakiliwa video akicheza densi kwa furaha katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na bendera ya Tanzania begani.

Alipokelewa kwa furaha na mamake bibi harusi Iyabo Ojo ambaye pia ni mwigizaji maarufu nchini Nigeria.

Mwingine aliyewasili Tanzania kwa ajili ya harusi hiyo ni Prince Enioluwa Adeoluwa ambaye ni rafiki wa karibu wa bibi harusi Priscilia kati ya wengine wengi.

Wanandoa ambao pia ni wanamuziki wa Tanzania Nandy na Billnass walitangaza kwamba wao ndio watakuwa wasaidizi wakuu wa maharusi katika hafla ya kesho.

Juma Jux na Priscilla wameandaa hafla kadhaa za ndoa nchini Nigeria na nchini Tanzania ya kesho ikiwa ya mwisho ambayo wameipa jina la “JP2025 Grand Finale”.

Share This Article