Dadake marehemu Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga aitwaye Beryl Achieng ameaga dunia, familia ya Odinga imethibitisha.
Ruth Odinga ambaye pia ni dadake Raila alitoa tangazo la kifo cha Beryl kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, bila kuelezea kilichosababisha kifo hicho.
Alisema wamekubali mapenzi ya Mungu katika kuondokewa ghafla kwa Beryl ambaye ameacha watoto watatu ambao ni Ami Auma, Chizi na Taurai lakini hakusema lolote kuhusu mume wa mwendazake.
“Ingawa tunahuzunishwa sana na kifo chake na pengo kubwa aliloliacha katika maisha yetu, tunapata faraja kwa kuamini kwamba yuko salama mikononi mwa Bwana na tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya thamani ya muda tuliobarikiwa kuwa naye na kwa athari kubwa aliyokuwa nayo kwa wote waliomfahamu,” aliandika Ruth.
Kifo cha Beryl kinajiri yapata mwezi mmoja na siku kadhaa baada ya taifa la Kenya kumpoteza Raila Odinga ambaye aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu.