Mwanamuziki maarufu wa mtindo wa R&B Craig David atatumbuiza katika awamu ya pili ya tamasha la World of Sounds, litakalofanyika Agosti 29, 2025 katika bustani ya hoteli ya Sheraton jijini Kampala nchini Uganda.
Awamu hiyo ya mwaka huu ya tamasha hilo, itaangazia muziki wa R&B na jioni hiyo itakuwa ya kipekee ya muziki wa hisia, sanaa ya kuvutia, na maonyesho ya utamaduni wa hali ya juu.
Craig David, mwimbaji, mtunzi wa nyimbo na mtayarishaji kutoka Uingereza anayejulikana kwa nyimbo kama “7 Days”, “Fill Me In” na “Walking Away” atakuwa jukwaani nchini Uganda kwa mara ya kwanza.
Uwepo wake katika tamasha hili unatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya muziki mwaka huu na ni tukio la kihistoria kwa jiji la Kampala.
Katika miaka zaidi ya ishirini ya kazi yake, Craig David ameuza zaidi ya rekodi milioni 15 duniani kote na ameteuliwa mara kadhaa kuwania tuzo za BRIT na Grammy, akichangia kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa mitindo ya UK garage na R&B.
Tamasha la World of Sounds lilianzishwa mwaka 2023 katika Hoteli ya Serena jijini Kampala na liliwavutia watazamaji kwa orodha ya wasanii wa kuvutia akiwemo mpiga gita maarufu wa mtindo wa afro-jazz Myko Ouma na Jose Sax, Sewa Sewa, Kenneth Mugabi na onyesho la kushtukiza la duet na Juliana Kanyomozi.
Baada ya mafanikio hayo, awamu ya pili ya tamasha hili inaleta uzoefu wa hali ya juu zaidi, kwa kujumuisha Craig David kama msanii mkuu wa kimataifa.
Tamasha hili pia litajumuisha wasanii bora wa muziki wa moja kwa moja na wapiga vyombo wa Uganda, likiahidi mchanganyiko wa kipekee wa vipaji vya kimataifa na vya ndani.