COTU yataka Mchina aliyedhulumu mfanyakazi afurushwe

Marion Bosire
2 Min Read
Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli.

Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini COTU unataka raia wa Uchina aliyenaswa kwenye video akidhulumu mfanyakazi wake raia wa Kenya afurushwe kutoka Kenya.

Katika taarifa iliyotolewa leo Novemba 16, 2025, COTU ililaumu mchina huyo kwa kuhujumu haki na hadhi ya wakenya huku ikitaka uchunguzi utekelezwe dhidi ya waia wa kigeni wanaotumia vibaya madaraka yao nchini.

Video ya tukio hilo imesambaa mitandaoni nchini kwa siku kadhaa na inaonyesha mwajiri huyo akimfokea mfanyakazi husika ndani ya kile kinachoaminika kuwa bohari jijini Eldoret.

Mchina huyo aliyeonekana kupandwa na hasira alichukua bati moja kutoka kwa mabati yaliyokuwa katika eneo hilo na kumpiga mfanyakazi huyo kwalo.

Video hiyo ilighadhabisha wengi wa watumizi wa mitandao ya kijamii nchini Kenya, wengi wakitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mwajiri huyo.

Katika video hiyo, mfanyakazi anayedhulumiwa anaonekana kujikaza zana na kujizuia asije akampiga mwajiri wake huku sauti ikisikika ikimwambia ajibu kipigo hicho lakini hakufanya hivyo.

Baadaye ilibainika kwamba jamaa huyo tayari amemsamehe mkubwa huyo na wameridhiana, maridhiano ambayo wengi wanatilia shaka mitandaoni wakihisi kwamba huenda alishurutishwa kumsamehe.

Picha ya wawili hao wakisalimiana kwa mikono imesambaa mitandaoni leo Jumapili ikifuatiwa na video ya maridhiano kati yao.

Mkenya husika anasikika kwenye video hiyo akisema kwamba tayari amemsamehe bosi wake na kwamba atasalia kuwa mfanyakazi wake. Anasikika kwenye video hiyo akizomea wakenya ambao huenda wasikubaliane na hatua yake ya kumsamehe bosi wake.

Share This Article