Nancy Nnadi ambaye wengi wanamjua kama Coach Nancy na ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya muziki ya EeZee Conceptz amebatilisha rasmi usemi wake uliomharibia sifa mwimbaji wa nyimbo za injili Mercy Chinwo Blessed.
Coach Nancy alitangaza hayo kupitia akaunti yake rasmi ya Instagram Jumapili akielezea kwamba aliafikia uamuzi huo kufuatia ushauri wa wakili wake.
“Kufuatia ushauri wa wakili wangu na kwa ajili ya amani na upendo wa Mungu, ninabatilisha chapisho langu la awali kuhusu Mercy Chinwo” aliandika Nancy.
Aliendelea kusema kwamba anaomba Mungu akamilishe mchakato unaoendelea wa kuafikia ukadiri kati ya Chinwo na EeZee Conceptz unaoendeshwa na wahubiri wakuu nchini Nigeria.
Hatua ya Nancy inajiri miezi kadhaa baada ya Mercy Chinwo, kupitiwa kwa mawakili wake wakiongozwa na Pelumi Olajengbesi, kuwasilisha kesi katika mahakama kuu ya Abuja dhidi ya Nancy kwa kumchafulia jina mteja wao.
Leo mawakili hao wa kampuni ya Law Corridor wametoa taarifa rasmi ya kutambua hatua aliyochukua Nancy ya kubatilisha aliyoyasema awali.
“Tunatambua na kukaribisha ubatilisho wazi uliotolewa na Nancy Nnadi almaarufu Coach Nancy, mkurugenzi mtendaji wa EeZee Conceptz Limited, kuhusu maneno ya kuchafua jina aliyoyasema awali kuhusu Mercy Chinwo Blessed” ilisema taarifa hiyo ya mawakili wa Chwinwo.
Kulingana nao suala hilo sasa limetatuliwa kikamilifu baada ya Nancy kutimiza masharti yaliyojumuisha kufuta ujumbe aliochapisha na kuubatilisha hadharani.
Mercy Chinwo anaripotiwa kupokea ubatilisho huo kwa unyenyekevu na neema na kwa moyo wa upendo na msamaha.