Chuo cha Zetech chamuenzi GG Kariuki

Marion Bosire
2 Min Read

Chuo kikuu cha Zetech kimetoa heshima kwa marehemu aliyekuwa mbunge wa Laikipia Godfrey Gitahi Kariuki, ambaye wengi walimfahamu kama GG Kariuki, kutokana na mchango wake kwa sekta ya elimu.

Taasisi hiyo ya elimu ya juu imezindua bamba la kumkumbuka Kariuki katika bewa lake la Mang’u na kutangaza mipango ya kujenga kituo kitakachoitwa “Dr G.G. Kariuki EGH” katika maktaba yake.

Mwanawe Kariuki aitwaye James Waigwa Kariuki, alipokea heshima hiyo kwa niaba ya familia yake katika bewa la Mang’u la chuo kikuu cha Zetech.

Waigwa alipongeza taasisi hiyo kwa kutambua athari aliyokuwa nayo babake na kujitolea kwake kupanua upatikanaji wa elimu hasa katika maeneo ya mashinani ya kaunti ya Laikipia.

Alibainisha kwamba babake alitoa rasilimali zake binafsi kama ardhi, kwa ajili ya ujenzi wa taasisi za masomo.

Mwanawe GG Kariuki aliongeza kuwa familia inaendeleza urithi alioujenga wa babake ambao wakazi wengi wa Laikipia bado wanautambua kama ishara ya maendeleo na fursa.

GG Kariuki, alikuwa Mbunge wa kwanza wa Laikipia wakati wa uhuru mwaka 1963, alitekeleza jukumu muhimu katika kuunda mwelekeo wa maendeleo ya kaunti hiyo.

Anasifika sana kwa kupigania elimu na kuboresha maisha katika eneo hilo.

Alichangia pakubwa katika kuanzishwa kwa shule nyingi za upili kama Rumuruti, Ngumo, Gatero Girls, Mwenje, Njorua, na Njonjo Girls.

Pia aliunga mkono uundaji wa shule kadhaa za msingi kama vile Rumuruti, Kiguro na Waigwa.

Kando na elimu rasmi, marehemu alihamasisha maendeleo ya ujuzi kwa kusaidia kuanzisha vituo vya mafunzo ya ufundi vya Igwamiti, Rumuruti, Kinamba na Muthengera, ambavyo vinawezesha vijana kupata utaalamu muhimu wa kiufundi.

Share This Article