Chimezie afurahikia athari aliyokuwa nayo kwa Davido

Hii ni baada ya Davido kukiri kwamba wimbo wa Bright Chimezie uitwao 'Because of English' ulimchochea kuandika na kuimba wimbo 'With You' ambao amemshirikisha Omah Lay.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria Bright Chimezie amedhihirisha mapenzi na heshima aliyonayo kwa mwanamuziki mwenza Davido akisema anafurahia kwamba alimmotisha katika muziki.

Hii ni baada ya Davido kukiri kwamba wimbo wa Bright Chimezie uitwao ‘Because of English’ ulimchochea kuandika na kuimba
wimbo ‘With You’ ambao amemshirikisha Omah Lay.

“Najivunia kwamba nilimmotisha Davido” alisema mwanamuziki huyo mkongwe katika mahojiano.

Chimezie hata hivyo alisema kwamba alishtuka wakati Davido alifichua athari aliyokuwa nayo katika muziki wake.

“Maneno hayawezi kuelezea ninavyojihisi. Nimefurahi sana. Nahisi nimeheshimishwa. Ninamshukuru Davido kwa kutambua kwamba alimotishwa na wimbo wangu” aliendelea kusema mzee huyo.

Chimezie alisema kwamba kabla ya ufichuzi wa Davido, hakuwa na ufahamu kuhusu uhusiano kati ya wimbo wake na ule wa Davido.

“Yeye ndiye alinielewesha hilo. Alinipigia simu akakiri kwamba alimotishwa na wimbo wangu” alisema Chimezie akiongeza kwamba alishangazwa na unyenyekevu wa Davido.

Gwiji huyo wa muziki alionekana kwenye video ya wimbo huo wa Davido na Omah Lay.

Anasema kinyume na wanamuziki wengine wakongwe walioachia vijana tasnia ya muziki, yeye bado anaimba hasa baada ya kutia saini mkataba na kampuni ya Sony kuhusu usambazaji wa kazi zake.

Share This Article