Mama Taifa Rachel Ruto mapema wiki hii,alizindua mpango wa Bustani za Chakula Nyumbani almaarufu Mama Kitchen Gardens, lengo kuu likiwa kuhakikisha utoshelevu wa chakula nchini na kuwaimarisha kina mama kiuchumi.
Mama Taifa anasema Bustani hizo za Chakula Nyumbani zitahakikisha jamii zinapata vyakula vilivyo na virutubishi na hivyo kutokomeza utapiamlo hasa miongoni mwa watoto.
Wazo hilo limeungwa mkono kikamilifu na kina mama wengi huku baadhi yao hata wakianzisha bustani hizo nyumbani kwao.
Bustani za Chakula Nyumbani zinapiga jeki ajenda ya serikali ya Kenya Kwanza ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha kote nchini.
Miongoni mwa wale ambao wamelikumbatia wazo hilo na kulitekeleza kikamilifu ni Naibu Msemaji wa serikali Mwanaisha Chidzuga. Mwanahabari huyo wa kupigiwa mfano anasema bustani hizo za chakula na matunda nyumbani ni muhimu sio tu ili kuimarisha jamii kiafya bali pia kiuchumi.
Chidzuga aliandamana na Mama Taifa Mei 14, 2025 kuzindua rasmi mpango wa Bustani za Chakula Nyumbani katika kaunti ya Baringo. Mwanahabari huyo ambaye ni mzaliwa wa kaunti ya Kwale, anasema Bustani za Chakula Nyumbani hazina gharama kubwa kuzianzisha kwa kuwa zinatumia vifaa vinavyopatikana nyumbani kama vile chupa za plastiki, magurudumu ya magari na magunia, miongoni mwa vingine.
“Sio lazima kuwe na ardhi kubwa kuanzisha bustani hizi. Kina mama wanaweza kuzianzisha kupitia vifaa vinayopatikana hapa nyumbani na pia hazina gharama kubwa. Bustani hizi zitawezesha kupatikana kwa utoshelevu wa chakula nyumbani na hata shuleni,” aliungama Chidzuga.

Kupitia mpango huo unaoongozwa na Mama Rachel, Chidzuga ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa shule ya msingi ya Ziwani, kaunti ndogo ya Matuga, kaunti ya Kwale anasema jamii zitaweza kupata fedha za ziada kutokana na mauzo ya mboga na matunda kutoka kwa Kitchen Gardens, huku fedha hizo zikitumika kununua vyakula ambavyo havipatikani nyumbani na kuhakikisha afya bora.
“Nawapongeza sana kina mama wa hapa nchini kutokana na bidii yao ya mchwa. Kupitia mpango huu, unaweza ukapata hela zako za ziada kutokana na kuwauzia majirani mboga. Utapata mia mbili au mia tatu yako na itakusaidia pakubwa,” alisema Chidzuga.
Chidzuga aliyasema hayo wakati akikagua Bustani za Chakula, tabasamu yake ya kipekee ikiashiria tosha manufaa makubwa ya mashamba haya madogo ya mboga na matunda. Moja ya manufaa hayo imetajwa kuwa kusaidia katika kukabiliana na dhuluma dhidi ya wanawake.
Huku visa vya dhuluma za kijinsia vikiripotiwa katika sehemu kadhaa hapa nchini, Chidzuga anasema Bustani za Chakula Nyumbani zitasaidia mno kuvipiga dafrau visa hivyo, ikizingatiwa kuwa kina mama sasa watakuwa na hela mfukoni.
“Kitchen Gardens zitasaidia kukabiliana na dhuluma dhidi ya wanawake. Ikiwa utapata fedha kutoka hapa, utauliza mtu pesa ya chumvi au za sodo? La hasha! Utaweza kujikimu. Mpango huu ni mzuri, natumai kina mama tutaukumbatia kwa haraka sana,” aliongeza Naibu Msemaji huyo wa serikali.

Uhifadhi wa mazingira ni suala muhimu linalopewa kipaumbele nchini Kenya. Bustani za Chakula Nyumbani zinafanikisha uhifadhi wa mazingira kupitia kuzuia utupaji taka ovyo. Chidzuga anasema kupitia mradi huu, sio lazima kutupa vifaa vya plastiki, mifuko ya dukani, nguo kuukuu na magurudumu, akidokeza kuwa vyote hivyo vitatumika katika kuanzisha bustani hizo za chakula nyumbani.
“Taka nyingi ni za plastiki. Ukimaliza kutumia mifuko ya plastiki, badala ya kutupa kwenye taka, jaza mchanga nenda katika maduka yetu ya kuuza mbegu na pande pale,” alishauri.
Chidzuga aliyesomea katika shule ya upili ya Kenya High, Nairobi, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Moi, amewasihi Wakenya hasa kina mama kukumbatia Bustani za Chakula Nyumbani kutokana na manufaa yake ya kumezewa mate.
Rais William Ruto alimteua Mwanaisha Chidzuga kuwa Naibu Msemaji wa serikali Oktoba 1, 2025, wadhifa anaoushikilia hadi sasa.
Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh ambaye anaongoza wizara hiyo katika kufanikisha mpango wa Mama Kitchen Gardens, alisema lengo la mpango huo ni kuwa na Bustani za Chakula milioni mbili, katika familia na shule milioni moja kote nchini.