Mshindi wa nishani ya shaba ya Olimpiki mwaka 2024, katika mbio za mita 3,000, kuruka viunzi na maji Faith Cherotich, atazindua uhasama dhidi ya watesi wake wa mwaka jana katika mkondo wa tatu wa mashindano ya Diamond League leo usiku mjini Doha, Qatar.
Cherotich aliye na umri wa miaka 20, atapambana na bingwa wa Olimpiki Winfred Yavi wa Bahrain, na mshindi wa nishani ya fedha ya Olimpiki Peruth Chemutai wa Uganda.
Bingwa wa zamani wa dunia kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20,katika mita 3,000, Teresia Gateri, atashirikiana na Susan Ejore na Nelly Chepchirchir katika mita 1,500.
Bingwa mara mbili wa mita 800, katika michezo ya Jumuiya ya Madola Wycliff Kinyamal, atajitosa uwanjani pamoja na Wakenya wenza Aaron Cheminingwa, na Laban Korir, katika shindano la mizunguko miwili.
Bingwa wa Dunia kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20,mwaka jana Reynold Cheruiyot atatimka mita 5,000 pamoja na wenzake Boaz Kiprugut na Cornelius Kemboi.
Aliyekuwa bingwa wa Dunia mwaka 2015, Julius Yego, pia atafungua msimu wa urushaji sagai mjini Doha leo.
Mshindi wa dhahabu tatu za Olimpiki na 10 za dunia, Shelly Ann Fraser Pryce wa Jamaica, atakimbia mita 100 kwa mara ya kwanza tangu ajiondoe katika nusu fainali ya Olimpiki mwaka jana.