Mshindi wa nishani ya shaba ya Olimpiki Faith Cherotich, atakuwa akiwinda ushindi wa tatu wa Diamond League, msimu huu atakaposhiriki mita 3,000 kuruka viunzi na maji, katika mkondo wa Paris,Ufaransa leo usiku.
Cherotich ambaye pia ni mshindi wa nishani ya shaba ya dunia, alitwaa ushindi katika mkondo wa Doha Mei 16 akiweka muda wa kasi ulimwenguni, kabla ya kushinda tena mjini Oslo Juni 12,akipiga tena muda wa kasi.
Bingwa huyo wa zamani wa dunia kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20, anaongoza msimamo dunia kwa alama 16 ,akifuatwa na bingwa wa Olimpiki Winfred Yavi kutoka Bahrain kwa pointi 14.
Hata hivyo Cherotich, atakabiliana na bingwa wa Olimpiki mwaka 2021 Peruth Chemutai wa Uganda, na Mkenya mwenza Caren Chebett.
Susan Ejore wa Kenya anayeongoza msimamo na mwenzake Nelly Chepchirchir watashiriki mita 1,500 .
Jacob Krop na Boaz Kiprugut, watajitosa katika mita 5,000, wakitoana jasho na mshindi wa nishani ya fedha ya dunia Yomif Kejelcha wa Ethiopia, anayeongoza msimamo wa dunia kwa pointi 25.
Wycliff Kinyamal na Nicholas Kiplangat watakimbia mita 800, huku bingwa wa zamani dunia Julius Yego akishiriki urushaji sagai.