Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Huduma za watoto Hanna Wendot Cheptumo, amelaani vikali kisa cha kudhulumiwa kwa mwanamke aliyetambuliwa kuwa Bella Comedy, wakati wa sherehe ya Kutit kwenye mkahawa wa Carnivore mwishoni mwa wiki.
“Nimeitazama video hiyo ya kuhuzunisha. Tunalaani vikali dhuluma zozote dhidi ya wanawake na wasichana,” alisema Waziri Cheptumo.
“Visa kama hivyo so tu uhalifu lakini pia vinakiuka haki na uhuru kuambatana na katiba ya taifa hili. Haki za wanawake ni haki za binadamu,” aliongeza waziri huyo.
Cheptumo alimhakikishia mwathiriwa huyo na umma kwa jumla kwamba wizara yake inashirikiana na asasi za usalama, kuhakikisha swala hilo linachunguzwa na wahasiriwa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wakati huo huo waziri huyo alitoa wito kwa waandalizi wa sherehe na wamiliki wa maeneo ya burudani kuhakikisha viwango vya juu vya usalama na ulinzi kwa wote wanaoshiriki.
Cheptumo alitoa wito wa ushirikiano wa pamoja katika kutokomeza dhuluma dhidi ya wanawake hapa nchini.