Chebet, Kipyegon, Wanyonyi na Odira warejea kutoka Tokyo

Dismas Otuke
1 Min Read

Mabingwa wa Dunia Faith Kipyegon, Beatrice Chebet, Lillian Odira na Emmanuel Wanyonyi wamerejea nyumbani leo kutoka Tokyo, Japani, walikoshiriki mashindano ya Riadha Duniani.

Familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na maafisa wa serikali walijitokeza kuwapokea mashujaa hao katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Wakizungumza punde baada ya kutua JKIA, Kipyegon na Chebet walisema wanaazimia kusalia katika mbio za uwanjani kabla ya kuhamia barabarani.

“Nafurahia sana kushinda dhahabu ya nne katika mbio za mita 1,500 na pia kuwamotisha kina dada wengine kwa sababu mimi ni kama mama yao. Beatrice amekuwa akitazama nikikimbia, na saa hii tunakimbia naye,” alisema Kipyegon.

Aidha, Chebet amesema anaangazia kushinda medali zaidi katika mita 5,000 na 10,000, huku akisema ushirikiano wa kikosi cha Kenya ulichangia matokeo.

Odira amesema anajipanga sasa kushiriki mashindano ya Ultimate mwaka ujao baada ya kutwaa ubingwa wa Dunia.

Kenya ilimaliza ya pili katika msimamo wa nishani kwa dhahabu 7, fedha 2 na shaba 2.

 

Share This Article