Chebet na Kipyegon waanza Diamond League kwa ushindi

Dismas Otuke
2 Min Read

Mabingwa wa Olimpiki Faith Kipyegon na Beatrice Chebet wamefungua msimu wa Diamond League kwa mikogo wakisajili ushindi na muda wa kasi ulimwenguni katika mkondo wa Xiamen nchini China leo.

Chebet alitimka mita 2,000 za mwisho akishinda mbio za mita 5,000 kwa muda wa dakika 14 sekunde 27.12, akifuatwa na Gudaf Tsegay aliyewaongoza Waethiopia kuchukua nafasi za pili hadi saba.

Bingwa mara tatu wa Olimpiki katika mbio za mita 1500 alikosa kuvunja rekodi ya dunia ya mita 1,000 kwa mara ya tatu akikata utepe kwa dakika 2 sekunde 29.21 ukiwa muda wa kasi duniani.

Abbey Cladwell and Sarah Billings wa Australia walimaliza katika nafasi za pili na tatu kwa dakika 2 sekunde 32.94 na dakika 2 sekunde 33.95 mtawalia.

Mwanariadha mwenye kasi ulimwenguni Ferdinand Omanyala, amemaliza wa pili kwa mara ya pili msimu huu akitumia sekunde 10.13, nyuma ya Akani Simbine wa Afrika Kusini aliyetwaa ubingwa kwa sekunde 9.99.

Simon Kiprop na Edmund Serem walimaliza katika nafasi za tatu na nne katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji nyuma ya Samuel Firehu wa Ethiopia, aliyeibuka mshindi kwa dakika 8 sekunde 5.61, akifuatwa na bingwa wa Dunia na Olimpiki Soufiane El Bakkali kutoka Morocco kwa dakika 8 sekunde 6.66.

Mkondo wa pili wa Diamond League utaandaliwa Mei 3 mjini Shanghai, China.

Share This Article