Changan yazindua safu kamili ya chapa na ubunifu wa NEV katika maonyesho ya Auto Shanghai 2025

Eric Biegon
4 Min Read
Kampuni ya Changan Automobile ilionyesha safu ya bidhaa zake kamili kwenye maonyesho ya Auto Shanghai 2025. Picha/Changan Automobile

Maonyesho ya Auto Shanghai 2025 yalifunguliwa Aprili 23, huku kampuni maarufu ya Changan Automobile ikivutia umakini mkubwa baada ya kuzindua safu ya bidhaa zake mbalimbali, hii ikiwa ni pamoja na ubunifu wake wa hivi punde wa magari mapya ya nishati safi (NEVs) kwa zaidi ya vyombo vya habari 600 na washirika 500 wa kimataifa.

Wakati wa hafla hiyo, kampuni hiyo iliyo na makao yake makuu jijini Chongqing, iliweka bayana mafanikio yake ya hivi karibuni na mikakati ya baadaye kupitia miradi yake mikuu mitatu: “Shangri-La Plan” kwa ajili ya nishati mpya, “Dubhe Plan” kwa teknolojia ya akili ya kuendesha, na “Vast Ocean Plan” kwa upanuzi wa kimataifa. Bidhaa zake tatu maalum — yaani CHANGAN, AVATR, na DEEPAL — pia zilionyesha bidhaa zao za hivi punde.

AVATR, chapa ya magari mapya ya nishati ya Changan ya kiwango cha juu, ilionyesha AVATR 06 iliyozinduliwa hivi karibuni, pamoja na mifano mingine, ikiwa ni pamoja na AVATR 07, 11, na 12. Mifano hii inatumia teknolojia ya kuendesha kupitia akili unde ya hali ya juu na ina muundo wa kipekee.

Wakati huo huo, DEEPAL, inayolenga watumiaji vijana na wenye ufahamu mzuri wa masuala ya teknolojia, ilizindua SUV yake ya kwanza iliyoboreshwa ya DEEPAL S09. Mfano huu unachanganya mtindo, usalama, na uzoefu wa kuendesha wa kusisimua, huku ukidhihirisha uwezo wa kampuni hiyo wa kuwapa thamani wateja wake.

Wakati wa hafla hiyo, mwenyekiti wa Changan Automobile, Zhu Huarong, alitangaza kuwa kampuni hiyo “itazindua bidhaa 45 mpya kote duniani katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwa na lengo la kuuza magari milioni tano (5) ifikapo mwaka 2030.”

Mwaka uliopita wa 2024, CHANGAN ilipata mauzo ya magari 536,000 nje ya nchi, ikionesha ukuaji wa mwaka kwa mwaka wa asilimia 47.9 na kujihakikishia nafasi miongoni mwa wauzaji wakubwa watatu wa magari kutoka China.

Songvit Titipoonya, Mkurugenzi Mtendaji wa Eternity at One, AVATR, na msambazaji wa DEEPAL nchini Thailand, alidokeza kuwa wanunuzi 500 wa kwanza wa gari aina ya AVATR walikuwa wafuasi wa zamani wa bidhaa maarufu za Kijapani na Kihispania. Uzoefu wao mzuri na magari ya nishati mpya (EV) ya hali ya juu umesababisha kuenea kwa maoni chanya, kuhusiana na gari hilo la AVATR wenye sifa na hadhi ya juu katika soko la Thailand.

Lee Barret, ambaye ni mtengenezaji wa vipindi kutoka Uingereza, hivi karibuni alitembelea kiwanda cha CHANGAN kilichoko Nanjing na kuhudhuria mkutano wake wa uzinduzi. Akitoa maoni yake kuhusu magari ya umeme kutoka China, alisema, “Nadhani magari ya Ulaya yako nyuma kwa kiasi fulani yakilinganishwa na bidhaa za nishati mpya kutoka China. Bidhaa za Kichina katika miaka michache iliyopita zimepiga hatua kubwakatika ubora na teknolojia, na nadhani ni baadhi ya magari bora zaidi duniani sasa.”

Kama sehemu ya mkakati wake wa kuhakikisha ukuaji wenye ubora zaidi, kampuni ya CHANGAN imejumuisha maendeleo endelevu katika shughuli zake za kimsingi. Kuorodheshwa kwake kwenye orodha ya “China ESG Listed Companies Pioneer 100” kunasisitiza kujitolea kwa kampuni hiyo kutimiza malengo ya mazingira, kijamii, na usimamizi (ESG).

Kusonga mbele, kampuni ya CHANGAN inapanga kuwekeza zaidi ya yuan bilioni 200 (takriban dola za Marekani bilioni 27.43) katika kipindi cha mwongo mmoja ujao ili kujenga mfumo wa teknolojia ya magari ya kizazi kijacho. Mpango huo unajumuisha kupanua kikosi chake cha utafiti kwa kuongeza wataalam 10,000, kuendeleza utengenezaji wa magari ya roboti za kisasa, kupima magari yanayopaa ifikapo mwisho wa mwaka huu, na kuzindua roboti za kibinadamu ifikapo mwaka 2028.

Share This Article