Mabingwa watetezi Senegal, almaarufu Teranga Lions, watashuka uwanjani Amaan kisiwani Zanzibar leo Jumanne usiku kukabiliana na Nile Crocodiles kutoka Sudan, katika mechi ya mwisho ya kundi D kuwania kombe la CHAN.
Pambano hilo litapigwa kuanzia saa mbili usiku huku mshindi akifuzu kwa robo fainali.
Sudan wanaongoza kundi hilo kwa alama 4 sawia na Simba wa Teranga walio na uhaba wa magoli.
Ni sharti Senegal washinde ili kufuzu kwa robo fainali ilihali sare itafuzisha timu zote endapo Nigeria itawashinda Congo au watoke sare pia.

Congo maarfufu kama Red Devils ni lazima washinde Nigeria katika mechi hiyo itakayoandaliwa uwanjani Benjamin Mkapa ili kufuzu kwa robo fainali.
Washindi wa kundi D watachuana na Algeria kwenye robo fainali ya Jumamosi huku timu ya pili ikiwa na miadi dhidi ya viongozi wa kundi C, Uganda Cranes katika robo fainali.