Serikali itaimarisha usalama zaidi katika mechi ya pili ya Kenya ya kundi A kuwania kombe la CHAN Alhamisi hii dhidi ya Angola, kuanzia saa moja usiku katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.
Kikao cha usalama kiliandaliwa Jumanne na Katibu wa Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, kamati andalizi ya CHAN ikiwakilishwa na Rais wa Shirikisho la FKF, Hussein Mohammed, Katibu katika Wizara ya Michezo Elijah Mwangi, na msimamizi wa mashindano ya Shirikisho la Kandanda Afrika, CAF, Nasser Khaled.
Dkt. Omollo ametoa hakikisho kuwa usalama utaboreshwa zaidi kwa mashabiki watakaohudhuria mechi ya Alhamisi usiku.
Haya yanajiri wakati kulikuwa na visa kadhaa vya utovu wa usalama wakati wa mechi ya ufunguzi kati ya Kenya na DRC Jumapili iliyopita katika uwanja wa Kasarani.
Baadhi ya mashabiki walijaribu kuvunja lango nambari 6 katika uwanja wa Kasarani na kuingia bila kulipa, huku baadhi ya wageni wengine wakiwemo wabunge na maseneta wakitaka kuingia uwanjani kupitia mlango unaotumiwa na Rais.