Mwanamuziki wa Uganda Jose Chameleone alirejea nyumbani jana kutoka nchini Marekani ambako amekuwa kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita kwa ajili ya matibabu.
Nguli huyo wa muziki alipokelewa na mashabiki wengi pamoja na watu wa familia yake katika uwanja wa ndege wa Entebbe.
Akihutubia wanahabari, Jose alifichua kwamba atarejea Marekani katika muda wa wiki chache zijazo kwani anastahili kuendelea na matibabu kutokana na ukweli kwamba hajapona kabisa.
Mmiliki huyo wa kampuni ya muziki ya Leone Island alisafirishwa hadi Marekani Disemba mwaka 2024, kwa ajili ya matibabu bora.
Mwimbaji huyo anaonekana buheri wa afya lakini ameelezea kwamba anahitaji matibabu na ufuatiliaji zaidi.
“Nimerudi kwa sababu nimetamani nyumbani na ninahitaji kuwa hapa, lakini nitarejea Marekani kama tarehe 2 Mei kwa ajili ya ufuatiliaji.” alisema Jose Chameleone.
Alisema anatumia dawa za bei ghali mno ziitwazo ‘Creon’ ambapo kipimo cha miezi mitatu pekee kinagharimu dola elfu 8 sawa na milioni moja pesa za Kenya.
Dawa hizo hutumiwa na watu ambao kongosho zao zimeathirika kiasi kwamba haziwezi kutoa vimeng’enya vya kutosha vya kumeng’enya chakula mwilini.
Kwa muda mrefu Jose Chameleone hakuwa amefichua ugonjwa unaomsibu huku akilazwa hospitalini mara kwa mara lakini mwanawe mkubwa alifichua kwamba anaugua ugonjwa wa kongosho uliosababishwa na matumizi yaliyopitiliza ya pombe.