Mwanamuziki anayeugua wa Uganda Jose Chameleone ametoa onyo kali kwa mtangazaji mmoja wa redio nchini Uganda baada yake kutoa habari za uongo kumhusu.
Mtangazaji huyo wa kituo cha redio cha ‘Radio 4’ aitwaye Janie Namukasa alidai kwamba Jose Chameleone amekamatwa na maafisa wa polisi kwa kumdhulumu mwenyeji wake huko Marekani Juliet Zawedde.
Lakini baadaye ilibainika kwamba maafisa walioonekana kwenye video wakimchukua Chameleone kutoka nyumbani kwa Zawedde ni wa usaidizi wa dharura na walikuwa wakimpeleka hospitalini baada ya kuzidiwa ghafla.
Jose alipelekwa hospitalini kwa ajili ya upasuaji wa kongosho.
Alifichua kwamba alitumiwa video ya Namukasa akitoa madai hayo ya uongo na Abitex mwandalizi wa matamasha na anasema ilimtamausha mno.
Amewataka watu wenye hulka kama ya Namukasa wakome kusambaza habari za uongo kwani vitendo vyao huenda vikawaweka pabaya.
Chameleone alichapisha video aliyorekodi akiwa hospitalini ya kuwasilisha ujumbe huo huku akihakikishia mashabiki wake kwamba anasubiri upasuaji na atawajuza kila kitu baada ya upasuaji.
Zawedde ndiye alimsafirisha Chameleone na kakake Weasel hadi Marekani mwezi Disemba mwaka jana baada ya Jose kuugua na kulazwa katika hospitali ya Nakasero jijini Kampala.