Chameleone aafikia ufanisi kwenye Mdundo

Kampuni ya kusambaza muziki mitandaoni ya mdundo hutambua wasanii wanaofanya vyema kila mara.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Uganda Joseph Mayanja au ukipenda Jose Chameleone ameafikia ufanisi mkubwa katika jukwaa la mitandaoni na muziki la Mdundo nchini humo.

Kulingana na chapisho la kampuni hiyo inayohusika na usambazaji wa muziki mitandaoni, Chameleone ameafikia kiwango cha Gold yaani dhahabu.

Hii ni baada ya kazi zake za sanaa kushushwa zaidi ya mara milioni 2.4 kutoka kwenye jukwaa hilo.

kakake Pius Mayanjamaarufu kama Palasso, naye ameafikia ufanisi huo ambapo kazi zake za muziki zimepakuliwa zaidi ya mara milioni 2.1.

Wasimamizi wa kampuni ya mdundo nchini Uganda walichapisha bango la kutangaza ufanisi huo kwenye Instagram ambapo walimtaja Chameleone huku wakimtakia msanii huyo afueni ya haraka.

Chameleone ambaye amefanyiwa upasuaji alioashiria kwamba ulifanikiwa hivi maajuzi, hajasema lolote kuhusu habari hiyo njema.

Jose Chameleone wa umri wa miaka 45 sasa, alianza kazi kama mpiga muziki yaani Dj mwaka 1996 jijini Kampala kabla ya kuhamia Nairobi ambako aliota mizizi kama mwanamuziki mwaka 1998.

Wakati huo alikuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya muziki ya Kenya iliyofahamika kama Ogopa Deejays, ambayo ilimsaidia kutoa wimbo wa kwanza uitwao ‘Bageya’ ambao alimshirikisha msanii Redsan wa Kenya.

Albamu yake ya kwanza kwa jina ‘Mama Mia’, ilizinduliwa mwaka 2000 na akawa na kasi ya juu ya kurekodi nyimbo ambapo kufikia mwaka 2013, alikuwa ametoa albamu 13.

Kazi zake zinazojulikana sana ni pamoja na Kipepeo, Shida za dunia, Valu valu, Bayuda, Badilisha, Sweet Banana na Champion.

Kwa sasa yuko nchini Marekani ambapo anapokea matibabu kutokana na matatizo ya kongosho.

Share This Article