Serikali ya Jamhuru ya kidemokrasia ya Congo DRC imesema imesimamisha chama cha Rais wa zamani Joseph Kabila, siku chache baada ya mali zake kuvamiwa na maafisa wa usalama.
Katika taarifa, wizara ya usalama wa ndani ya DRC ilisema kwamba uamuzi huo unafuatia uanaharakati uliozidi wa Kabila, aliyehudumu kama Rais kwa miaka 18 hadi mwaka 2019 na ambaye amesalia kuwa kiongozi wa chama cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD).
Wizara hiyo ilifafanua kwamba shughuli zote za chama cha PPRD aimesimamishwa katika sehemu zote za taifa hilo.
Chama hicho hata hivyo hakikujibu hatua hiyo mara moja.
Rais Felix Tshisekedi amemlaumu Kabila kwa kuandaa kile alichokitaja kuwa uasi na kuunga mkono makundi yanayojumuisha M23 ambalo linapigana na wanajeshi wa serikali mashariki mwa DRC.
Kabila wa umri wa miaka 53, aliondoka nchini DRC kabla ya uchaguzi wa Urais mwaka 2023,kulingana na msemaji wa familia yake.
Lakini Mapema Aprili katika ujumbe uliowasilishwa na wafanyakazi wake, alisema kwamba atarejea nchini humo siku ambayo hakuitaja kwa sababu nchi hiyo iko katika hatari.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinaashiria kwamba atawasili karibuni au tayari amewasili katika mji wa mashariki wa Goma.
Msemaji wa familia ya Kabila alisema Alhamisi kwamba maafisa wa usalama walitekeleza msako katika makazi ya Kabila yaliyo katika eneo la Mashariki la jiji la Kinshasa na mengine yaliyo jijini.
Wizara ya usalama wa ndani nchini DRC imemshtumu Kabila na chama chake kwa kudhihirisha hali ya kuwa na makosa, kuhusika na ukimya kuhusu uvamizi wa Rwanda.
Serikali ya DRC, wataalamu wa umoja wa mataifa na maafisa wa kimataifa wamesema kwamba kundi la M23 linaungwa mkono na Rwanda, ambayo imekanusha madai hayo.
Kundi hilo linahusika pakubwa katika mzozo unaokumba maeneo ya Mashariki ya DRC na sasa linadhibiti miji ya Goma na Bukavu.
Taarifa ya wizara ya usalama wa ndani nchini DRC ilisisitiza kwamba Kabila hajachagua upande wowotw katika maasi ya M23 na hajawahi kuyalaani.
Ililaani hatua ya Kabila kuchagua kuingia nchini DRC kupitia mji wa Goma ambao uko chini ya usimamizi wa adui.
Taarifa nyingine kutoka kwa wizara ya masuala ya haki ilisema kwamba kiongozi mkuu wa mashtaka ameekezwa aanzishe hatua za kisheria dhidi ya Kabila kwa uhusika wake na matendo ya M23.