Chama cha MDG chakabidhi wagombea Tiketi, Chataka IEBC kuendesha Uchaguzi huru na wa haki

Francis Ngala
2 Min Read

Chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) kinachoongozwa na Mbunge wa Ugenya Mhe. David Ochieng, hii leo kimekabidhi tiketi rasmi za uteuzi kwa wagombea wawili watakaowania nyadhifa katika chaguzi ndogo zijazo.

Waliokabidhiwa tiketi hizo ni Bw. Collins Okeyo Omondi, mgombea wa ubunge wa Eneo Bunge la Kasipul Kaunti ya Homa Bay,  na Bw. Joel Ongoro Otuoma, mgombea wa udiwani wa Wadi ya Kisa East. Hafla hiyo ilifanyika katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi, ikiongozwa na kiongozi wa Chama David Ochieng.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Ochieng alitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhakikisha kuwa uchaguzi unaoandaliwa unazingatia maadili ya uchaguzi na unafanyika kwa njia huru, ya haki, na kwa amani.

Kiongozi wa Chama cha MDG David Ochieng akimkabidhi Collins Okeyo Omondi tiketi ya kuwania kiti cha eneo bunge la Kasipul kupitia chama cha MDG

“Kama chama tunalaani vikali aina yoyote ya vurugu. Tunawasihi wagombea wote wajiepushe na vitendo vya uchochezi, waheshimiane na wazingatie sheria,” alisema Ochieng.

“Tunaitaka IEBC ichukue hatua kali dhidi ya wagombea wanaotumia vurugu kuwatisha wapinzani wao.”

Aidha alionya kuwa matukio ya hivi karibuni ya vurugu yaliyojitokeza wakati wa mchujo wa vyama kote nchini yanahatarisha misingi ya demokrasia na akasisitiza kuwa ni wajibu wa IEBC kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa maadili ya uchaguzi.

Kwa upande wake mgombea wa kiti cha ubunge cha Kasipul, Collins Okeyo Omondi alitilia mkazo umuhimu wa uchaguzi wa amani, huku akitoa wito kwa wapinzani kujiepusha na vitendo vya vurugu au uchochezi.

Alisisitiza kuwa yuko tayari kwa ushindani wa hoja na si wa vurugu, na akawahimiza wapiga kura kuwachagua viongozi wenye maadili na uwajibikaji.

Share This Article
Follow:
I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.