Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetoa vigezo ambavyo wagombea wanahitaji kuwa navyo kuelekea chaguzi ndogo zilizoratibiwa kuandaliwa Novemba 27 mwaka huu.
Chaguzi hizo zimeratibiwa kuandaliwa katika maeneo 24 ya uwakilishi kote nchini.
Miongoni mwa vigezo hivyo ni pamoja na: Mgombea anapaswa kuwa raia wa Kenya kwa kipindi kisichopungua miaka 10 kabla ya uchaguzi huo, asiwe na uraia pacha kabla ya kuingia madarakani, alipe ada ya kugombea wadhifa husika inayoanzia shilingi 2,500 hadi 50,000, na kuwa na orodha ya wafuasi wake ambayo inapaswa kuambatana nakala za vitambulisho za wafuasi hao.
IEBC inapanga kufanya chgauzi hizo ndogo baada ya waliokuwa wawakilishi wa maeneo husika ama kufariki au kuteuliwa serikalini.
Mathalan, uchaguzi mdogo utaandaliwa katika eneo bunge Malava Novemba 27 kufuatia kifo cha aliyekuwa mjumbe wa eneo hilo Malulu Injendi mapema mwaka huu.
Kwa upande mwingine, uchaguzi mdogo utaandaliwa katika eneo bunge la Ugunja baada ya aliyekuwa mjumbe wa eneo hilo Opiyo Wandayi kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati.
Vyama vya kisiasa vimo mbioni kuteua wagombea wao kuelekea chaguzi hizo zinazotarajiwa kuwa kipimajoto cha ubabe wa kiasiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.