Cardi B na Stefon Diggs huenda wameachana

Inakisiwa wameachana kufuatia hatua ya Cardi B ya kufuta picha zao za pamoja kwenye akaunti yake ya Instagram.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Cardi B huenda ameachana na mpenzi wake Stefon Diggs, kufuatia hatua yake ya kufuta picha zao zote za pamoja kwenye akaunti yake ya Instagram.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Cardi na mchezaji huyo wa mpira kuonyesha wazi kwamba wako kwenye mahusiano ya kimapenzi.

Mwanzo wa mwezi Juni mwaka huu wa 2025, wawili hao walichapisha picha za pamoja zilizowaonyesha wakiwa katika ziara nchini Ufaransa.

Kulingana na ripoti, Diggs alikuwa amekodisha kasri liitwalo Château de Farcheville karibu na jiji la Paris kwa gharama ya dola elfu 12, kwa usiku mmoja.

Kasri hilo lina chumba cha muziki, spa, eneo la mvinyo na maeneo mengine ya kifahari.

Diggs kwa upande wake hajafuta picha yoyote aliyowahi kuchapisha inayomwonyesha akiwa pamoja na Cardi na hali hiyo sasa inachanganya mashabiki wao wasiojua iwapo wameachana au la.

Uvumi kuhusu wawili hao kuwa kwenye mahusiano ulijiri mwisho wa mwaka 2024, baada yao kuonekana pamoja jijini New York na huko Miami.

Mwezi februari mwaka huu wa 2025 walionekana tena pamoja na kuzidi Kuchochea tetesi za kuwa wapenzi. Aprili 2025 Cardi alionekana akisakata densi mbele ya Diggs katika eneo moja la burudani baada ya tamasha la Coachella.

Mei 2025 walihudhuria mchezo wa mpira wa kikapu ambapo timu ya New York Nicks ilikuwa ikicheza. Walikuwa wakishikana mikono na kuonyeshana mahaba na hivyo kuthibitishia umma kwamba ni wapenzi.

Juni Mosi, Cardi B alichapisha picha kadhaa zilizomwonyesha yeye na Diggs wakijifurahisha kwenye Yatch.

Share This Article