Cardi B akubali mpango wa kushangaza wa kuachana na Offset

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa mtindo wa rap nchini Marekani Cardi B anaripotiwa kukubali mpango wa kushangaza wa kugawana mali anapotafuta kuachana na baba ya watoto wake na mwanamuziki mwenza Offset.

Ripoti zinaashiria kwamba Cardi ambaye aliwasilisha ombi la talaka Septemba 2024, aliamua kukubali mpango huo kutokana na hali ya sasa ya kuwa na ujauzito wa mwanaume mwingine huku akiwa mke wa Offset.

Cardi B amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mchezaji wa mpira Stefon Diggs na wanatarajia mtoto wao wa kwanza hatua ambayo ingefanya kesi ya talaka iwe ngumu zaidi.

Offset alidai wagawane mali katika kiwango cha asilimia 70 kwake na asilimia 30 kwa Cardi ikitizamiwa kwamba alimwacha na watoto akaenda kuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine na sasa wanatarajia mtoto.

Kawaida watu wengi hugawana mali katika kiwango cha asilimia 50 kwa asilimia hamsini.

Utajiri wa Cardi B unaripotiwa kuwa wa jumla ya dola milioni 100 na wa Offset ukiwa dola milioni 40, na iwapo kweli wamekubaliana kugawana mali katika kiwango cha asilimia 70/30, Cardi atampa Offset zaidi ya dola milioni 50.

Cardi B na Offset walikuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka 7 na wana watoto watatu Blossom wa umri wa mwaka mmoja, Wave wa miaka minne na kifungua mimba Kulture wa miaka minane.

Ndoa yao ilijaa misukosuko ambapo mara kwa mara Cardi B alidai kwamba Offset hakuwa mwaminifu na alimwambukiza magonjwa ya zinaa.

Share This Article