Mwanamuziki wa Marekani Cardi B alikuwa mahakamani Jumanne Agosti 26, 2025 kujitetea katika kesi ambayo anadaiwa kushambulia mwanamke aliyekuwa mlinzi mwaka 2018.
Cardi B ambaye jina lake halisi ni Belcalis Almanzar alitoa ushahidi wake katika kesi hiyo ambapo alisema kwamba vita kati yake na mlinzi huyo wa kike siku hiyo vilikuwa vya maneno tu.
Alisema alikuwa anatembea kwenye afisi ya Daktari fulani huko Beverly Hills akiwa na ujauzito wa miezi minne siku hiyo na mlinzi huyo kwa jina Emani Ellis,akawa anamfuata akimrekodi video akitumia simu yake.
Mwanamuziki huyo anasema alilazimika kumfokea Ellis wakajibizana wakitupiana maneno makali likiwemo neno “Bitch” lakini kamwe hawakupigana.
Ellis alikuwa ameambia mahakama Jumatatu kwamba Cardi B alimshambulia na kumng’ata kwenye shavu la kushoto na kucha na hivyo kumuacha na jeraha.
Cardi hata hivyo alisisitiza kwamba hawakupigana kwani Ellis ana mwili mkubwa kuzidi wake na hangejaribu kupigana naye akachagua kumrushia maneno tu.
Msanii huyo hata hivyo alikiri kwamba hakuona video au picha alizompiga Ellis siku hiyo hata ingawa anaamini kwamba alimrekodi au kumpiga picha.
Ellis mkazi wa Los Angeles aliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya Cardi mwaka 2020 akidai kwamba alishambuliwa na mwanamuziki huyo ambaye alimpiga kichwani, usoni, akamtemea mate na akamtukana.
Kulingana naye, kucha ndefu za Cardi B zilimsababishia majeraha usoni hali iliyohitaji afanyiwe upasuaji wa kuimarisha sura yake.