Shirikisho la soka barani Afrika CAF limempa Rais William Ruto tuzo ya mafanikio ya kipekee kufuatia ufanisi wa mashindano ya CHAN 2024.
Haya yalifanyika katika tuzo za CAF za mwaka 2025 zilizoandaliwa nchini Morocco lakini Rais hakuwepo na tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba yake na balozi wa Kenya nchini humo Jessica Gakinya.
Tuzo hiyo ni utambuzi wa juhudi za serikali ya Kenya za kuimarisha michezo barani Afrika kupitia miundombinu na kutoa mfumo bora wa usaidizi kwa wanariadha.
Rais wa CAF Patrice Motsepe alisema kwenye hafla hiyo kwamba soka ya Afrika inahitaji ushirikiano kutoka kwa nchi nyingine ndiyo sababu kila mwaka wanatambua nchi zilizoshirikiana katika maendeleo ya soka.
Maandalizi ya pamoja ya kipute cha CHAN 2024 kati ya Kenya, Uganda na Tanzania ambayo yalifanikiwa ndiyo sababu kuu ya kutambuliwa kwa Rais Ruto na wenzake Samia Suluhu na Yoweri Museveni.
Serikali imekuwa pia ikijibidiisha kukarabati viwanja vya michezo nchini kwa lengo la kukuza vipaji zaidi hata katika maeneo ya mashinani.
Ilikarabati viwanja vya Nyayo na Kasarani na kuanzisha ujenzi wa uwanja wa michezo wa Talanta kwa gharama ya bilioni 45.
Uwanja huo wa Talanta utakaokuwa na nafasi ya mashabiki elfu 60, umekamilika kwa kiwango cha asilimia 66, ukitarajiwa kukamilika kabisa kufikia mwaka ujao.