Kipindi cha burudani katika sherehe za leo za siku kuu ya Madaraka katika kaunti ya Homa Bay kilikuwa cha kufana sana ambapo kilionyesha utamaduni wa jamii ya waluo.
Watoto ambao ni wanafunzi wa jumla ya shule 11 za msingi za Homa Bay walifungua kipindi hicho kwa michoro ya kusherehekea siku kuu ya Madarka wakitumia kauli mbiu “maji yetu Thamani yetu”.
Walianza kwa kuandika neno Homa Bay, kisha wakachora mashua huku wakiweka kitambaa cha samawati upande wa chini kuashiria maji na wakaghani shairi la kusifia juhudi za kukuza uchumi samawati.
Baadaye waliunda jina Blue Economy na kufoka “Maji Yetu thamani yetu” na katika shairi lao watoto hao waliendelea kusema kwamba ajira imeongezeka na utalii ukanawiri kutokana na juhudi za serikali za kukuza Uchumi Samawati.
Samaki pia haikusaazwa kwani watoto hao waliunda mchoro wake huku Bonny Musambi ambaye ni mkurugenzi wa uratibu katika Ikulu akitania kwamba kutokana na hatua ya Rais ya kupunguza bei ya unga wa ugali sasa mlo umekamilika.
Walipoondoka watoto hao, waliingia wanamuziki wakiwemo waimbaji na wacheza densi za Kitamaduni, wale wa mtindo wa Ohangla na wale wa nyimbo za injili.
Walitumbuiza kwa densi za kitamaduni kama Ramogi ya jamii ya luo, ile ya Irirandi Rya Basuba ya jamii ya Suba na Orutu iliyopatiwa jina la “Chop Inee Homa Bay Dala”.
Baada ya hapo waliingilia nyimbo za mtindo wa Ohangla ambazo ni pamoja na “Kenya Mor Tee” uliohusisha wasanii kama Othicho Jasuba, Aroji Chogo, Papa T, Freddy Jakadongo, Abongo Jakabwana, Achieng Nyarongo, Oluoch Digital, Kaka Talanta na Linda Owino.
Kibao kingine kilichopigwa ni “Tuwajibike” kilichohusisha wasanii kama Awicko Wuod Nyapala, Lizzy Seme, Lynder Matiko AKA Rhumba Queen, Eddah Ayon, Sherine Pammy, Omondi CEO, Kapweps Anto na Abungu System.
Waimbaji wa nyimbo za injili kama Christine Otieno, Phoebe Moses Aphy, Janet Oudu, Fred Omondi, Akowa Irene, Milka Omondi, MC Paul Otieno Oleche, Linda Owino, Kevin Gombe na Wuod Fibi walihitimisha kipindi hicho cha burudani kwa wimbo uliopatiwa jina la “Washindi”.