Burna Boy aomba msamaha kuhusiana na alichokifanya

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria ambaye pia ni mshindi wa Tuzo za Grammy, Dlamini Ebunoluwa Ogulu, maarufu kama Burna Boy, ameomba msamaha katika video mpya inayosambaa mitandaoni.

Kwenye video hiyo, anaonekana akitumbuiza jukwaani huko Texas na inaaminika amechukua hatua hiyo kufuatia mauzo duni ya tiketi za maonyesho yake, baada ya tukio la utata kwenye moja ya maonyesho yake.

Anajitetea akisema kwamba alichokifanya kilitokana na kuteleza kwa ulimi wake na kwamba hakumaanisha alichokisema.

Tatizo lilianza wakati wa onyesho la Burna Boy huko Denver, Colorado, nchini Marekani aliposimamisha tumbuizo lake baada ya kugundua shabiki wa kike akiwa anasinzia akiwa ameketi kwenye safu ya mbele.

Mwimbaji huyo alitaka shabiki huyo aondolewe kabla ya kuendelea kuimba, akimtaka mpenzi wa msichana huyo amtoe au onyesho lenyewe likomeshwe kabisa.

Tukio hilo lilighadhabisha wanamitandao kote ulimwenguni, hali iliyozidi kuwa mbaya baada ya video ya zamani inayomuonyesha Burna Boy akisema kuwa anapenda mashabiki matajiri na kwamba hamwombi mtu yeyote amuunge mkono ikiibuliwa tena.

Baada ya ukosoaji mkubwa mtandaoni, mashabiki wengi waliripotiwa kususia maonyesho yake, jambo lililosababisha mauzo duni ya tiketi katika vituo mbalimbali vya ziara.

Burna Boy anaripotiwa kufutilia mbali baadhi ya maonyesho yake kwenye ziara yake inayoendelea ya “No Sign of Weakness” nchini Marekani.

Onyesho la Novemba 28, 2025, katika ukumbi wa The Armory huko Minneapolis, lilifutwa siku moja kabla ya siku ya tukio hilo, kulingana na Ticketmaster, sawa na onyesho lake la Chicago, lililopangwa kufanyika Desemba 1, 2025.

Share This Article