Bunge limetangaza kwamba Rais William Samoei Ruto atahutubia kikao maalum cha pamoja cha bunge la kitaifa na bunge la Seneti siku ya Alhamisi, Novemba 20, 2025, kuanzia saa 8:30 mchana.
Tangazo hilo limetolewa kwa pamoja na Spika wa bunge la kitaifa, Moses Wetang’ula na Spika wa bunge la Seneti, Amason Kingi, kwa mujibu wa Kifungu nambari 132 sehemu ya kwanza (b) cha Katiba, kinachomtaka Rais kuhutubia kikao maalum cha bunge angalau mara moja kila mwaka.
Kulingana na taarifa hiyo, kikao hicho kitaandaliwa katika ukumbi wa bunge la kitaifa, jengo kuu la bunge, jijini Nairobi.
Inatarajiwa kwamba hotuba ya Rais itagusia mafanikio makuu ya serikali, vipaumbele vya sera na ajenda ya kisheria kwa mwaka ujao.
Kikao hicho maalum kimeitishwa kufuatia taarifa rasmi kutoka kwa Rais Ruto kwa Maspika wa mabunge yote mawili. Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za bunge, wanachama na umma wanatakiwa kufahamishwa tarehe, muda na mahali pa kikao hicho.
Hii itakuwa ni hotuba ya kila mwaka ya Rais kwa bunge la kumi na tatu katika kipindi chake cha nne, jukumu la kikatiba linalosisitiza uwajibikaji wa serikali kuu kwa bunge na taifa kwa ujumla.